Ligi Kuu

Mechi ya Pamba yampa mzuka kocha Yanga

MWANZA:KOCHA  Mkuu wa Yanga, Hamdi Miloud, amesema kuwa ana mkakati maalum kwa ajili ya kuhakikisha timu yake inapata alama tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji FC.

Yanga tayari imewasili Mwanza kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Ijumaa, Februari 28, katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Miloud amesisitiza kuwa kikosi chake kimejiandaa kikamilifu kwa ajili ya pambano hilo.

“Kesho tunacheza dhidi ya Pamba, na tumejipanga kwa mtazamo ule ule kama ilivyo kwa michezo mingine. Tutafanya kila linalowezekana kushinda kwa sababu alama hizi ni muhimu kwetu,” alisema Miloud.

Hata hivyo, kocha huyo amesema hana uhakika na mbinu zitakazotumiwa na Pamba Jiji FC, lakini anafahamu kuwa wapinzani wao wataingia uwanjani kupambana kwa nguvu ili kubaki kwenye ligi.

“Sijui kama Pamba wamejiandaa vya kutosha, lakini najua wanahitaji alama hizo. Ikiwa mimi ningekuwa kocha wao, nisingetumia mbinu nyepesi kwa sababu wanapambana kusalia ligi.

Timu hii ilitoka sare dhidi ya Singida Black Stars, jambo ambalo si rahisi. Wanaweza kushambulia na kufunga, lakini na sisi tuna mkakati wetu wa ushindi. Hata hivyo, siwezi kuweka wazi mbinu zetu kwa sasa kwa sababu ni siri ya mchezo,” aliongeza.

Miloud amesisitiza kuwa Yanga haipo Mwanza kwa likizo, bali kwa kazi moja tu—kushinda.

“Tunaiheshimu Pamba, lakini tupo hapa kwa ajili ya ushindi na hatutaki kingine zaidi ya alama tatu. Tunajua mchezo hautakuwa rahisi, lakini tuko tayari kupambana,” alisema.

Kocha huyo pia alizungumzia namna ambavyo timu pinzani hucheza kwa kujituma zaidi zinapokutana na Yanga.

“Kila timu inapocheza dhidi ya Yanga inatoa kila kitu. Tunatarajia mchezo mgumu, lakini tunapaswa kuthibitisha kuwa sisi ni timu kubwa,” alisema Miloud.

Kuhusu mashabiki, kocha huyo raia wa Tunisia alieleza kuvutiwa na uungwaji mkono anaoupata kutoka kwa Wanayanga.

“Nina uzoefu mkubwa wa soka barani Afrika na nimefanya kazi na klabu kubwa, lakini mashabiki wa Yanga ni wa kipekee.

Wanapokuja kwa wingi kutuunga mkono, wanatupa motisha kubwa ya kupambana zaidi,” alihitimisha.

Related Articles

Back to top button