Crazy Kennar kufanya onesho Desemba 14
NAIROBI: MCHEKESHAJI wa Kenya, Crazy Kennar ameweka wazi kwamba onesho lake la vichekesho la ‘Happy Country 2024’ litafanyika Kasarani Arena mnamo Desemba 14 mwaka huu.
Kennar amesema malengo ya onesho hilo ni kupata watazamaji 4,000 huku akigusia kusikitishwa na kumkosa mtoto wake ambaye alitamani angekuwa sehemu ya onesho lake hilo atakaloliendesha kwa muda wa saa mbili kabla ya dakika 5 za mapumziko.
Kennar amesema mtoto huyo alimpata na mke wake Natalie Asewe, lakini aliaga dunia baada ya kukaa kwa siku tano katika chumba cha wagonjwa mahututi (NICU) na walitamani angekuwa hai ili awe sehemu ya onesho hilo kwa sababu mtoto huyo alifariki wakati baba yake alikuwa akiandaa kipindi cha uchekeshaji ambacho atakionyesha siku ya onesho lake.
“Nilitakiwa kuja hapa kama baba, lakini kwa bahati mbaya mwanangu alifariki siku nne zilizopita. Imekuwa moja ya wakati mgumu zaidi maishani mwangu, nikikabiliana na maumivu hayo huku nikiandaa kipindi,” ameeleza.
Kennar pia amechukua fursa hiyo kuhimiza huruma miongoni mwa watu. “Kila unapoona mtu akitabasamu, chukua muda muulize kama yuko sawa. Tuwe walinzi wa kaka na dada zetu, tupendane maana kuna mambo mengi sana katika Maisha ya mwanadamu,” alihimiza.
Natalie Asewe, kwenye mtandao wake wa Instagram, ameandika kumbukumbu za dhati kwa marehemu mtoto wao wa kiume, aliyefariki dunia Desemba 11. Akishiriki picha ya ujauzito wake, alitafakari uchungu wa kufiwa na mtoto na ndoto ambazo hawakuwahi kuzitimiza.
“Wanasema hakuna uchungu zaidi kuliko kuzaa, lakini sikubaliani. Maumivu makubwa zaidi ni kubeba mimba na kujifungua mtoto ambaye hujawahi kumlea. Sihuzunikii mwanangu tu bali nyakati ambazo hatutawahi kushiriki Pamoja, sijaona kilio chake cha kwanza, hatua zake za kwanza, sauti yake na wala sikumuoana akikua,” ameandika kwa huzuni mkubwa.
Kama mmoja wa wacheshi na waundaji wa maudhui mashuhuri barani Afrika, Kennar anaendelea kazi yake ya uchekeshaji na maisha yake binafsi. Kwa sasa anaishi Kenya na Afrika Kusini, ambapo anaongeza ujuzi kwa muda wa miaka mitatu.