
DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Mavokali amefunguka kuhusu changamoto nzito alizopitia katika safari yake ya muziki, akieleza kuwa aliwahi kufikia hatua ya kutaka kukata tamaa na kuachana kabisa na muziki kutokana na maumivu na dhuluma alizokutana nazo.
Mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na wimbo wa Commando amesema kwa kipindi cha takribani miaka miwili mfululizo amepitia nyakati ngumu zilizomuumiza kimya kimya huku akikabiliwa na vikwazo mbalimbali kwenye kazi yake ya muziki.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Story, Mavokali amesema awali aliamini kuwa kupata umaarufu na kufahamika kungekuwa suluhisho la matatizo yake, lakini mambo yalibadilika baada ya mafanikio kwani ndipo changamoto zilipozidi.
“Ndani ya miaka miwili iliyopita nimepitia maumivu, changamoto, dhuluma na vikwazo vingi kwenye muziki wangu. Kulikuwa na nyakati za kukata tamaa, nyakati za kuumia kimya kimya na nyakati ambazo nilihisi kama kila kitu kinaenda kinyume na mimi. Lakini pamoja na yote hayo bado nipo hapa,” ameandika Mavokali.
Aidha, msanii huyo amesema kuendelea kwake kuwepo kwenye muziki si kwa uwezo wake pekee bali ni kwa rehema na ulinzi wa Mwenyezi Mungu.
Mavokali ameongeza kuwa safari hiyo imemfundisha kwamba mafanikio hayaondoi vita vya maisha, bali wakati mwingine huwa mwanzo wa mitihani mikubwa zaidi.
“Naamini bado kuna sababu ya ndoto yangu kuendelea kuishi,” ameandika.




