Rapa Ice Prince amkana muigizaji Moet Abebe

LAGOS, Nigeria: RAPA maarufu wa Nigeria Ice Prince, amemkana muigizji Moet Abebe aliyedai kuwa katika uhusiano na rapa huyo na amemchumbia kwa miaka 12.
Prince amedai kwamba hayuko tayari kuwa katika uhusiano wa kujitolea kama alivyotangaza Moet kwamba amemchumbia kwa miaka hiyo yote.
Moet Abebe alidai wakati wa mahojiano kwamba yeye na Ice Prince wamekuwa kwenye uhusiano kwa miaka 12 huku tetesi zikiwa kwamba kunatuhuma za uhusiano nje ya mahusiano hayo.
Katika mahojiano na mtandao wa The DateBizz, rapa huyo alipinga madai yake, akisema kuwa kupata mapenzi imekuwa changamoto kwake na alivyoeleza Moet kuhusu yeye si sawa.
“Hivi karibuni, imekuwa vigumu kwangu kupata upendo. Sio kwa sababu sitaki, lakini akili yangu haijtulia kwa uhusiano. Na sitaki kuwa na msichana atakayeteseka kwa ajili yangu. Nahitaji kuweka sawa mambo yangu kwanza ikiwemo muziki wangu na masuala ya kipato ndipo nifikilie masuala ya mahusiano kwa sasa Hapana,” alifafanua Ice Prince na kuongeza;
“Ukiniona na mwanamke atakuwa mtu ninamheshimu sana, mtu ambaye tunaelewana. Mwanamke yeyote ambaye nimetoka naye kimahusiano ninamuheshimu mno mimi si mtu wa kucheza na hisia za wanwake,” alisema.