Mapenzi yamng’oa kambini mshiriki BSS

DAR ES SALAAM: MMOJA wa washiriki wa Shindano la Vipaji Bongo Star Search (BSS), Abiud Onesmo aliyefanya vizuri kati ya washiriki 20 bora, ametangaza kujiengua katika shindano hilo kwa madai ya shinikizo kutoka kwenye familia yake.
Licha ya madai hayo baadhi ya washiriki wenzake wanadai kuondoka kwa Abiud kunatokana na mwanamke wake kutoona faida ya mshiriki huyo kuendelea kuwa kambini wakati akiwa mtaani uingiza kati ya laki 3 hadi 5 kwa siku.
Mshiriki huyo alizua hofu baaada ya kutoonekana katika onyesho la wiki iliyopita ambapo washiriki wengine wote walipanda jukwaani na kuonyesha uwezo wao lakini mshiriki Abiud hakuonekana jukwaani.
Maneno ya washiriki wenzake:
Charles Burton ambaye ni mshiriki kutoka Dar es Salaam amemwelezea Abiud kuwa ni mtu asiyeshaurika walijitahidi kumshauri asiondoke lakini ameondoka na sababu ni mwanamke wake alidai anaumwa lakini alipofika nyumbani kwake alisema haumwi bali ‘alimmis’.
Mshiriki kutoka John Mwasomola Kutoka Arusha amesema walishauriana na Abiud ili asiondoke kambini baada ya kueleza sababu yake: “Abiud alikuwa akienda mtaani anarudi kwa mke wake akiwa na laki 5 mkononi sasa alipokuwa kambini wiki nzima hakuna kuingiza fedha ya hakumtumia mke wake… anaona mashindano kama kubet anaweza ashinde ama asishinde,
“Mke wake ameona kwa siku Abiud alikuwa akimleta kati ya laki 3 na 5 akaona bora mwanaume wake arudi…Tulimwambia asiondoke lakini ameamua kuondoka,”
Mshiriki kutoka Dar es Salaam Saluh Kulwa ameshangazwa na kuondoka kwa Abiud akidai kulikuwa na umuhimu wa kuwa na mtu kama huyo katika mashindano hayo makubwa kwa sababu hakuwa na sababu muhimu ya kumfanya aondoke mashindanoni.
Baada ya kueleza sababu za kujiondoa katika shindano hilo wadau na mashabiki walionyesha kugawanyika kwani wapo waliokerekwa na kujitoa kwake huku wakidai kwamba majaji walijua hilo lingeweza kutokea ndiyo maana walimtaka aache umapepe wakati anapofanya shoo, huku wengine wakimtakia mafanikio mema kutokana na kuwa na kipaji kikubwa.
Awali majaji wa shindano hilo Master J, 2kizzy na Madam Ritha walimfurahia mshiriki huyo huku wakimpongeza kwa kujua kutumia sauti yake katika uimbaji lakini walimtaka achake kuchachawa ‘mapepe’ wakati anaimba lakini baada ya ushauri huyo mshiriki huyo hajarudi tena jukwaani kuonyesha kama alikubali ushauri huo ama la.