Mahaba yambakisha Guardiola Etihad

MANCHESTER: Kocha mkuu wa Manchester city Pep Guardiola amesema uwamuzi wake wa kuoongeza mkataba kama meneja wa klabu hiyo kwa misimu miwili zaidi unatokana na upendo wake kwa klabu na mazingira mazuri yaliyowekwa na uongozi wa klabu hiyo.
Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 53 angemaliza mkataba wake wa sasa Julai 1 mwaka ujao kabla ya mabingwa hao wa Premier League kutangaza kumuongezea mkataba mpya wa miaka miwili siku ya Alhamisi.
“Si juzi wala jana, tangu kuanza kwa msimu huu nimefikiria mengi sana, nataka kuwa mkweli nilisema msimu huu nataka uwe wa mwisho lakini kuna nyakati tofauti tofauti na matatizo yanayotokea siku za hivi karibuni nikahisi kabisa huu sio muda sahihi wa kuondoka, nisingetaka kuiangusha klabu yangu naipenda”
“Angeweza kuja meneja mwingine yeyote na akafanya kazi nzuri kwa sababu mifumo ipo, uongozi upo na sapoti ipo lakini kwakuwa naipenda Manchester city nikaona kwanini nisisalie hapa” – amesema Pep.
Uamuzi wa Guardiola wa kuongeza muda wake Etihad ni muhimu kwa Man City wakati huu wababe hao wakisubiri hatma ya ikiwa wataadhibiwa baada ya kushtakiwa kwa makosa 115 ya ukiukaji wa kanuni za Ligi, mashtaka ambayo klabu hiyo inakanusha vikali.
Guardiola aliwasili Etihad 2016 na tangu wakati huo ameiongoza kutwaa mataji sita ya Ligi Kuu ya England, huku manne ya mwisho yakifululiza ikiwa ni rekodi kwenye Ligi hiyo. Pep pia aliiongoza City kutwaa mataji matatu ya kombe ligi, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa mwaka 2023.