Kompany: Kane msubirini kwanza

MAINZ: Licha ya Mfungaji kinara wa Bayern Munich Harry Kane kurejea mazoezini kocha wake Vincent Kompany amesema hatamjumuisha Mwingereza huyo katika mchezo dhidi ya Mainz kesho Jumamosi.
Vinara hao wa Bundesliga walichapisha video kwenye mitandao yao ya kijamii siku ya Alhamisi ikimuonyesha Kane, ambaye alipata jeraha la nyama za paja wakati wa sare ya 1-1 mwezi uliopita dhidi ya Borussia Dortmund, akifumania nyavu kwenye mazoezi ya mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo wa ugenini dhidi ya Mainz.
“Harry Kane hatacheza dhidi ya Mainz, wala wachezaji wengine walio majeruhi. Waliocheza dhidi ya Shakhtar Donetsk watacheza mechi hii”
“Kuangalia historia ya majeruhi ndani ya kikosi ni muhimu. Jukumu letu ni kuwapunguza. Hadi sasa tumefanikiwa kufanya hivyo, lakini tusishangae kwamba kuna wakati kunakuwa majeruhi kadhaa,” Kompany aliwaambia wanahabari.
Bayern, wenye kumbukumbu ya kushinda 5-1 dhidi ya Shakhtar Donetsk kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne, watawakosa pia Joao Palhinha, Alphonso Davies, Serge Gnabry na golikipa Manuel Neuer.