Kocha Yanga hana presha ya kuwepo nafasi ya pili

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga, Hamdi Maloud, amesema hana wasiwasi na timu yake kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani hiyo inawapa ari ya kupambana zaidi ili kuifikia nafasi ya kwanza.
Akizungumza baada ya Yanga kushika nafasi ya pili kwa pointi 46, huku Simba wakiwa kileleni kwa alama 47, Maloud alisema “Nafasi ya pili inatufanya tupambane zaidi kuifikia ya kwanza. Kuwa kileleni kuna changamoto kubwa, kwani kila timu inapambana kwa nguvu dhidi yako.”
Kocha huyo pia alizungumzia umuhimu wa kuboresha safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha wanatumia vyema nafasi wanazopata. Alikiri kuwa kwenye mechi yao dhidi ya JKT Tanzania walishindwa kuzitumia nafasi walizotengeneza, hivyo wanajipanga kurekebisha hilo kwenye mazoezi kuelekea mechi zijazo.
“Mechi ya JKT Tanzania, tulipata nafasi hatukuweza kuzifanyia kazi, tunarejea uwanja wa mazoezi kufanyia kazi kuelekea mechi zilizopo mbele yetu,” amesema.