Kiungo Zesco mambo safi Msimbazi

ZAMBIA: KLABU ya Simba imekamilisha dili la kumsajili kiungo mkabaji wa Zesco United ya zambia, Kelvin Kapumbu kutua katika viunga vya Msimbazi kwa msimu ujao wa mashindano.
Imeelezwa kuwa watu maalum waliotwikwa jukumu ya usajili wapo nchini Zambia kwa ajili ya kukamilisha dili la kiungo huyo kuongeza nguvu kwa wekundu hao wa Msimbazi kuongoza nguvu.
Taarifa zilizofika katika dawati la kachero wetu jana zinaeleza kuwa, kila kitu kimeenda vizuri kati ya mchezaji huyo na uongozi wa Simba na makubaliano ya miaka miwili.
“Mzambia, Kapumbu msimu ujao ni nyekundu na nyeupe, dili lake na Simba limeenda vizuri, usajili huu ni mapendekezo ya benchi la ufundi pamoja na mahitaji ya timu yetu baada ya mapungufu,” kimesema chanzo chetu cha kuaminika.
Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amesema kuanzia msimu ujao utakuwa wa furaha kwa sababu tajiri ameingia kazini.
“Agosti mwaka huu tutakuwa na furaha sana, tunafanya usajili mzuri na mambo yakienda vizuri basi kila wanasimba ataona na kusikia wachezaji, niwaombe wanasimba watulie mambo mazuri yanakuja, ” alisema Ahmed.