Kisa Red Bull, Mashabiki wa Dortmund wamnunia Klopp

UJERUMANI:MUDA mchache baada ya kocha wa zamani wa Liverpool Jurgen Klopp kutangazwa kuwa msimamizi mkuu wa shughuli za soka katika kampuni ya Red Bull, ambayo inamiliki klabu za RB Leipzig ya Ujerumani, RB Salzburg ya Austria, Red Bull Bragantino ya Brazil na RB New York ya Marekani, mashabiki wa Borussia Dortmund wamemvaa kocha huyo na kumuita msaliti.
Mashabiki hao ambao wengi wanaonekana kutofurahishwa na kitendo cha Klopp kukubali ofa hiyo kutoka kampuni ya vinywaji ya Red Bull ya nchini Austria wamevamia kurasa za mitandao ya kijamii ya kampuni hiyo na baadhi ya machapisho yanayohusu kutangazwa huko kwa Klopp na kushusha matusi.
Mashabiki hao wanamlaumu Klopp kwa ‘usaliti’ wa kujiunga na kampuni ya wapinzani wao kwenye Bundesliga kwa kuhofia huenda uwepo wake kwenye kampuni hiyo kutadhoofisha maendeleo ya Borussia Dortmund ambayo aliifundisha kabla ya kutimkia Liverpool.
Klopp aliyedumu Dortmund kwa miaka saba, amesaini mkataba wa ‘muda mrefu’ ambao kwa mujibu wa taarifa una nafasi ya kumruhusu kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani ikiwa atataka.
Kabla ya kukubali ofa hiyo Klopp amekuwa kwenye mapumziko baada ya kumaliza safari ya miaka 9 ya kuifundisha Liverpool mwisho wa msimu uliopita.
Kwa upande wa kampuni ya Red Bull inasema Klopp hatahusika katika shughuli za kila siku lakini atazishauri timu kuhusu falsafa, mkakati wa uhamisho na maendeleo ya ukufunzi. Klopp, raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 57 ataanza jukumu hilo tarehe 1 Januari 2025.