Kikapu

Kikapu Zanzibar wapata viongozi

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu Zanzibar (BFZ), imemtangaza Sabri Mohammed Muumin kuwa Rais wa shirikisho hilo atakayeongoza kwa miaka minne.

Sabri alitangazwa kushika nafasi hiyo kwa kuwa mgombea pekee ambaye kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo hakupaswa kupigiwa kura.

Aidha, kamati hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Amiri Mussa Amiri iliwatangaza viongozi wengine ambao wameshika nyadhifa mbalimbali wakiwa nao ni wagombea pekee.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti awali ilikuwa na wagombea wawili ambao ni Mohammed Salum Khamis na Hassan Ramadhan Abdallah, aliyetangazwa ni Abdallah kushika nafasi hiyo baada ya mwenzake kujitoa.

Aidha, nafasi ya Katibu Mkuu ilichukuliwa na Abdallah Juma Abdallah na msaidizi wake ni Hassan Khamis Hamad wote walikuwa wagombea mmoja mmoja.

Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo kulikuwa na sintofahamu kuhusu akidi ya wajumbe ambao walidai kwa mujibu wa kanuni ni wasipungue 23 ambao ni zaidi ya nusu ya wajumbe wote ambao ni 46.

Sintofahamu hiyo ilimfanya mgombea nafasi ya makamu mwenyekiti kujitoa na wapiga kura walikuwa 19.

Hata hivyo, Mrajisi wa Vyama vya Michezo na Klabu, Abubakar Mohammed Lunda aliingilia kati na kulitolea maamuzi suala hilo ambapo alisema uchaguzi ungeahirishwa kama wajumbe ambao hawakufika wangekuwa na sababu za msingi.

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya wajumbe hao awali walisema hawana nauli za kuwafikisha kwenye mkutano na Baraza likachukua hatua ya kuwapelekea nauli lakini walichokifanya ni kugomea uchaguzi na kurejesha nauli hizo.

Related Articles

Back to top button