Tano zafuzu robo fainali Kikapu Dar

TIMU tano za kikapu zimefuzu hatua ya robo fainali Ligi ya mkoa wa Dar es Salaam baada ya kumaliza mzunguko wa mechi 30 zikiwa zinazoongoza kwa kufanya vizuri.
Zilizofuzu ni Dar City iliyomaliza kinara kwa pointi 57, UDSM Outsiders wa pili kwa pointi 55, JKT wa tatu kwa pointi 53 sawa na Savio katika nafasi ya nne na Srelio iliyoko nafasi ya nane kwa pointi 45.
Ambazo ziko kwenye nane bora zinasubiri kumaliza mzunguko wa mwisho ili kujiunga na wenzao ni Mchenga katika nafasi ya tano yenye pointi 50, ABC katika nafasi ya sita pointi 46 na Vijana katika nafasi ya saba kwa pointi 45.
Timu nane za juu ndizo zitakazoingia hatua hii ya mtoano ambapo kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama Cha Basketball Dar es Salaam Haleluya Kavalambi, michezo ya kufunga mzunguko itamalizika mwishoni mwa wiki hii.
Michezo ya hatua ya mtoano kwa timu nane itaanza kuchezwa kuanzia Oktoba 8, mwaka huu hadi Oktoba 31 atapatikana bingwa wa jumla ya Ligi hiyo.
Timu ambazo ziko hatarini kushuka daraja ni Kampala International University KIUT, Jogoo na Crows ziko kwenye mstari mwekundu.
Wachezaji wanaoongoza katika ufungaji bora ni wengi ila watatu wenye pointi nyingi ni Stanley Mtunguja wa Ukonga Kings mwenye pointi 539 akiongoza pia kwa kuchangia pasi za mabao kwa pointi 158 akifuatiwa na Amina Juma wa Mchenga Queens pointi 524 na pasi pointi 136 na nafasi ya tatu ni Jonas Mushi wa JKT pointi 512.