Nyumbani

Mbunge Chamazi kuwa mgeni rasmi fainali za Ligi ya Maveterani

DAR ES SALAAM: MBUNGE wa Jimbo la Chamazi, Abdallah Jafari Chaurembo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika fainali za Ligi ya Maveterani Tanzania zitakazofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, huku waandaaji wakijivunia mafanikio yaliyopatikana katika msimu wa kwanza wa mashindano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwakilishi wa mbunge huyo, Mussa Francis, amesema fainali hizo zitakazochezwa Jumapili zinatarajiwa kuvutia wadau mbalimbali wa michezo pamoja na nyota wa zamani wa soka walioshiriki mashindano hayo.

“Tunaomba mashabiki wa soka na wananchi wa Jimbo la Chamazi na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushuhudia fainali hizo, Mbunge wetu atakabidhi medali na kombe kwa washindi wa mashindano hayo,”amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Maveterani Tanzania na Ofisa wa Usalama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Hashim Abdallah, amesema msimu wa kwanza wa ligi hiyo umefanikiwa kuwakutanisha nyota wa zamani wa soka kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuimarisha mshikamano miongoni mwao.

Hashim amesema licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza, waandaaji wanajivunia kufanikisha ligi hiyo na kuweka msingi mzuri wa maendeleo ya soka la maveterani nchini huku akibainisha changamoto kubwa zilizojitokeza katika msimu huo zilihusisha gharama za uendeshaji, usafiri wa timu pamoja na ratiba za mashindano kutokana na msongamano wa matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Kwa mujibu wake, baadhi ya timu zilishindwa kutimiza ratiba zao kutokana na changamoto za usafiri, hali iliyoathiri mwenendo wa mashindano katika baadhi ya hatua.
Hata hivyo, amesema waandaaji wamejifunza mengi kutokana na changamoto hizo na tayari wanaanza maandalizi ya msimu ujao kwa lengo la kuboresha ratiba, usimamizi na mfumo wa mashindano.

Hashim amesema ligi hiyo ilishirikisha timu kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Iringa, Tabora, Shinyanga na Kilimanjaro, jambo lililoonesha mwitikio mkubwa wa wapenzi wa soka la maveterani nchini.

Ameshukuru wadhamini na wadau mbalimbali waliochangia kufanikisha mashindano hayo, akiwemo Mkwabi Supermarket, Zurri International, HKB Protection and Management pamoja na Azam Complex kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika uendeshaji wa mashindano.

Naye mwakilishi wa timu ya Baruti Veterans, Vicente Peter ambaye pia, ni mchezaji wa zamani wa Biashara, Mtibwa Sugar, Yanga na timu ya taifa amesema walipoteana zamani lakini mashindano hayo yamewakutanisha na kutamba kuwa kupitia timu yake ya Baruti anaamini itachukua ubingwa katika hatua inayofuata ya mashindano hayo.

Mwakilishi wa Simba Veterans Innocent Njovu amesema walikuwa wanaongoza katika hatua za awali kilichowatoa mapema ni kushindwa kusafiri kwenda Tabora kuwafuata wapinzani kutokana na ukata, akiahidi timu yao itajipanga vizuri kwa ajili ya mwakani .

Kwa upande wake, Wakili Revocatus Kuuli amesema michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga afya, kukuza urafiki na kuimarisha mshikamano wa kijamii, hivyo akawapongeza waandaaji kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa washiriki.

Kuuli alikuja kukabidhi Kombe kwa uongozi huo kwa ajili ya mchezo wa fainali utakaochezwa Jumapili. Pia, kitakuwa na Zawadi nyingine na medali. Mpaka sasa Kuna timu nne zinazowania ubingwa ambazo ni Yanga Veterans, Raja Veterans, Baruti na Uhuru kutoka Kilimanjaro.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button