Jarjou: Nitafunga mabao mengi

SINGIDA: BAADA ya kuibuka shujaa wa Singida Black Stars kwa bao lililoizamisha KMC kwa ushindi wa bao 1-0, mchezaji Lamin Jarjou ametuma salamu nzito kwa wapinzani wake akiahidi kuwa bado hajamaliza kazi na kwamba ataendelea kufunga mabao mengi zaidi.
Jarjou alikuwa nyota wa mchezo huo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Airtel, Singida, baada ya kufunga bao pekee la ushindi na kuihakikishia timu yake pointi muhimu, huku akiondoka pia na tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.
Akizungumza baada ya mchezo huo, aliwashukuru mashabiki kwa sapoti yao kubwa na kusisitiza kuwa ushindi huo ulikuwa wa muhimu kwa upande wao.
“Asanteni kwa kutuunga mkono. Nitaendelea kufunga mabao mengi zaidi mbele. Kwangu mimi matokeo yalikuwa muhimu.” Amesema.
Jarjou amesema furaha yake kubwa ni kuona Singida Black Stars inapata matokeo chanya, huku akieleza kuwa sasa macho yao yote yanaelekezwa kwenye mechi ijayo.
“Nimefurahi tumepata matokeo. Kipaumbele chetu ni mchezo ujao dhidi ya Mbeya City kwenye Kombe la Shirikisho.”
Kauli hiyo inaonesha wazi kuwa pamoja na ushindi dhidi ya KMC, Singida Black Stars tayari imehamishia nguvu zake kwenye vita inayofuata, huku Jarjou akiwa mmoja wa silaha kubwa zinazotarajiwa kubeba matumaini ya timu hiyo.




