Isarito: Mapenzi yasizidi ndoto

MSANII wa filamu nchini, Isarito Mwakalindile, ‘Isarito’, ameweka bayana kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na mwigizaji mwenzake, Jacqueline Wolper, huku akisisitiza kuwa hataki masuala ya mapenzi yaathiri ndoto na shughuli zake za kazi.
Akizungumza kuhusu uhusiano huo, Isarito amesema yeye si mtu wa kuficha mahusiano yake, ingawa amekataa kuweka wazi ni lini alianza uhusiano wa kimapenzi na Wolper.
Amesema: “Mimi mahusiano yangu huwa siyafichi, japo siwezi kusema ni lini nilianza kudate na Wolper.”
Katika mahojiano hayo, Isarito aliulizwa kama kuanzisha uhusiano na Wolper kumemletea changamoto na watu wa mitindo, hususan wale walio karibu na Rich Mitindo.
Akionekana kutotaka kuhusishwa na mjadala huo, Isarito alihoji maana ya swali hilo na kueleza kuwa yeye ni muigizaji anayehitaji kuvaa vizuri katika shughuli zake za kisanaa.
“Mbona sikuelewi? Watu wa mitindo wanatengeneza nguo au wanafanyaje? Mimi ni muigizaji, kwa hiyo masuala ya mitindo lazima nivalishwe ili nipendeze,” amesema.
Alipoulizwa kama Rich Mitindo haoni kinachoendelea, Isarito alijibu kwa kuuliza sababu za kumhusisha mtu huyo katika mazungumzo yao.
“Kwa nini tumuongelee Rich Mitindo? Mimi sina shida naye, kwa hiyo tukianza kumuongelea hapa haitakuwa sahihi. Itakuwa ni uongo, maana sisi ni wanaume hapa, tumuongelee Wolper tu,” amesema.




