Nyumbani

Fadlu: Tutapambania kila kombe msimu huu

DAR ES SALAAM: PUNDE baada ya kutua Tanzania, kocha mpya wa Yanga, Fadlu Davids amesema atapambana kuhakikisha Yanga inapigania kutwaa makombe yote inayoshiriki msimu huu.

Fadlu aliyewahi kuinoa Simba SC ametua nchini usiku wa kuamkia leo Jumamosi kurithi mikoba ya Manqoba Mngqithi aliyetimuliwa hivi karibuni.

Licha ya Fadlu kueleza kusikia faraja kutua Tanzania kwa mara nyingine, lakini akafafanua namna anavyotaka kuirejesha Yanga kwenye makali yake na kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo.

“Yanga ilikuwa na mafanikio mazuri miaka mitano iliyopita, na tunataka kujenga na kuendeleza hayo mafanikio tena kwa kutengeneza namna ya kucheza, falsafa ya kucheza hatua kwa hatua, tutaboresha kikosi na kuifanya Yanga iwe imara kileleni.

“Niko hapa kwa ajili ya kutatua changamoto, na msimu haujawa mzuri mpaka sasa lakini tuna Ligi ya Mabingwa Afrika na michuano mingine na kila kitu kinawezekana,” alisema Fadlu.

Aidha, alikisifia kikosi cha timu hiyo kwa ubora wa wachezaji walionao, akieleza hatua kwa hatua ataingiza mbinu na aina mpya ya kucheza ambayo itawafurahisha na itawafariji mashabiki.

“Inafahamika Yanga inataka kushinda kila kombe, kwa hiyo hatutasimama kupambana kujaribu kushinda kila kombe tunalishiriki msimu huu,” alihitimisha Fadlu raia wa Afrika Kusini.

Aidha, Fadlu aliyewahi kuifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024-25 walipopoteza dhidi ya RS Berkane kwa mabao 3-1, amejiunga na Yanga akiwa huru baada ya kuachana na Raja Casablanca.

 

Related Articles

Back to top button