Filamu

Kasiga: Afrika kujifunza kutoka safari ya ‘Long March’

DAR ES SALAAM: KATIBU Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk. Gervas Kasiga, amesema Afrika inapaswa kujifunza misingi ya ujasiri, uvumilivu, mshikamano na kutokukata tamaa iliyobebwa na safari ya kihistoria ya ‘Long March’ nchini China ili kuimarisha juhudi za kufikia maendeleo na kujitegemea kiuchumi.

Dk. Kasiga ameyasema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanya na Shirika Kuu la Habari la China (CCTV), ambapo ameeleza namna hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping, ilivyompa tafakuri ya kina kuhusu historia ya safari hiyo na mafunzo yake kwa mataifa mbalimbali, hususan Afrika.

Katika mahojiano hayo, Dk. Kasiga amesema ameguswa na historia ya mapambano ya Jeshi Jekundu la China (Red Army), hasa namna lilivyokabiliana na changamoto mbalimbali wakati wa safari hiyo huku likidumisha imani, mshikamano na dhamira ya kufikia malengo yaliyokuwa mbele yao.

Amesema “Historia ya ‘Long March’ inatoa somo muhimu kwa mataifa ya Afrika kuhusu umuhimu wa kuwa na maono ya pamoja, uongozi wenye dhamira na mshikamano wa kitaifa katika kukabiliana na changamoto za maendeleo.

Aidha, amesisitiza kuwa “Mataifa ya Afrika yanapaswa kuchota ari na falsafa ya safari hiyo kwa kuimarisha umoja, uvumilivu na ujasiri katika kupambana na vikwazo vinavyokwamisha maendeleo na safari ya kujitegemea kiuchumi.

Ameeleza kuwa “Safari ya kihistoria ya China inathibitisha umuhimu wa kutokata tamaa katika kutekeleza malengo ya kitaifa, huku mshikamano na dhamira ya pamoja vikiwa nguzo muhimu katika kujenga mustakabali bora wa nchi.

Ushiriki wa Dk. Kasiga katika mahojiano hayo na CCTV ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, pamoja na kuimarisha mwonekano wa taasisi zake na viongozi wake katika mijadala inayohusu historia, utamaduni na mahusiano ya kimataifa.

Related Articles

Back to top button