Filamu

Mwigizaji mkongwe Tom Skerritt afariki dunia

NEW YORK: MWIGIZAJI mkongwe wa Hollywood, Tom Skerritt, aliyefahamika kupitia filamu maarufu zikiwemo Alien, MASH na Top Gun, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93.

Kwa mujibu wa taarifa ya familia yake, alifariki kwa sababu za kawaida, akiacha urithi wa kazi za uigizaji zilizodumu kwa zaidi ya miongo sita.

Familia yake ilieleza kuwa mbali na kutambuliwa duniani kupitia filamu, Skerritt alikuwa mcheshi, hekima, mdadisi na mkarimu. Pia alijali ubunifu, usimulizi wa hadithi, huduma kwa jamii, maveterani na utunzaji wa mazingira.

Skerritt alianza kupata umaarufu mkubwa mwaka 1970 kupitia filamu ya MASH, iliyoongozwa na Robert Altman. Katika filamu hiyo, alicheza nafasi ya Duke Forrest, daktari wa upasuaji wa Jeshi la Marekani wakati wa Vita vya Korea. Filamu hiyo ilipata uteuzi wa tuzo tano za Oscar.

Mwaka 1979, aliigiza nafasi ya Dallas, nahodha wa chombo cha anga, katika filamu ya kisayansi na hofu Alien, iliyoongozwa na Ridley Scott. Filamu hiyo iliyowashirikisha pia Sigourney Weaver na Ian Holm ilipata mafanikio makubwa na kuwa miongoni mwa kazi zenye ushawishi katika historia ya filamu za aina hiyo.

Mwaka 1986, Skerritt alionekana katika filamu maarufu Top Gun, akicheza nafasi ya Viper Metcalf, mwalimu wa marubani wa kijeshi. Filamu hiyo ilimshirikisha Tom Cruise na kuchangia kuimarisha umaarufu wake Hollywood. Skerritt pia alicheza katika filamu nyingine zikiwemo ‘Steel Magnolias’, ‘A River Runs Through It’, ‘Contact’ na ‘Tears of the Sun’.

Katika televisheni, Skerritt alijipatia umaarufu kupitia tamthilia ya Picket Fences, iliyokuwa hewani kuanzia mwaka 1992 hadi 1996. Aliigiza nafasi ya sherifu wa mji katika jimbo la Wisconsin na mwaka 1993 akashinda tuzo ya Emmy kama mwigizaji bora wa kiume katika tamthilia ya maigizo.

Skerritt alizaliwa Agosti 25, 1933, jijini Detroit, Marekani, na kabla ya kuwa mwigizaji alihudumu katika Jeshi la Anga la Marekani. Alianza safari yake ya filamu mwaka 1962 kupitia ‘War Hunt,’ ambamo aliigiza pamoja na Robert Redford. Katika maisha yake binafsi, alikuwa baba wa watoto watano na alifunga ndoa mara tatu.

Kifo chake kinaacha pengo katika tasnia ya filamu ya Hollywood, huku kazi zake zikiendelea kukumbukwa na mashabiki wa vizazi mbalimbali. Kwa zaidi ya miaka 60 katika filamu na televisheni, Skerritt alijenga historia ya uigizaji iliyomfanya kuwa mmoja wa waigizaji waliotambulika kwa uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali kwa mafanikio.

Related Articles

Back to top button