Billnass: Umri mpya, nyumba mpya na baraka mpya

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, William Lyimo ‘Billnass’, amegusa hisia za mashabiki baada ya kumwandikia ujumbe wa upendo mkewe, Faustina Mfinanga ‘Nandy’, katika siku yake ya kuzaliwa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Billnass amemtakia Nandy heri ya siku ya kuzaliwa huku akimwandikia ujumbe uliojaa upendo na baraka, akisema: “Umri mpya, nyumba mpya, baraka mpya.”
Aidha, msanii huyo amemuombea mkewe maisha yaendelee kumpa sababu nzuri za kuwa na furaha, huku akimueleza namna anavyompenda na kuthamini uwepo wake katika maisha yake.
Billnass ameshiriki ujumbe huo akiwa pamoja na Nandy nje ya nyumba mpya ya ghorofa, ambayo mwanamuziki huyo ameieleza kuwa zawadi aliyoamua kujizawadia katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa mwaka huu.
Kupitia video mbalimbali zilizosambazwa mitandaoni, Nandy ameonekana akiwa na furaha kubwa, akionyesha sehemu za nje na ndani ya nyumba hiyo mpya.
Wakati huo huo, ujumbe wa Billnass umeibua pongezi kutoka kwa mashabiki ambao, pamoja na kumtakia Nandy heri ya siku yake ya kuzaliwa, wamempongeza pia msanii huyo kwa namna anavyomuunga mkono mkewe katika hatua mbalimbali za mafanikio yake.
Baadhi ya mashabiki wameeleza kufurahishwa na jinsi Billnass anavyoonekana kusherehekea mafanikio ya Nandy tangu walipoanza uhusiano wao hadi walipofunga ndoa, wakitafsiri ujumbe wake kama ishara ya upendo na kuthaminiana katika maisha yao ya ndoa.




