Irene Uwoya: Mimi ni Malkia, Kajala anapenda kudeka

DAR ES SALAAM: MREMBO na msanii wa filamu za Bongo Movie, Irene Uwoya, amefunguka kuhusu tabia za baadhi ya mastaa wanaounda kundi lao, akidai kuwa yeye ni malkia wa kundi hilo huku Kajala akimtaja kuwa mtu anayependa kubembelezwa na kudekezwa.
Akizungumza kuhusu uhusiano wao ndani ya kundi hilo, Uwoya amesema kuwa pamoja na wakati mwingine kutofautiana, kugombana na kununiana, huwa wanajikuta wakirejea katika mazungumzo na kuendelea kuwa pamoja kama kawaida.
“Kwenye kundi letu unaweza kukutana tumegombana na tumenuniana wote, halafu ghafla tukajikuta tunaongea tu,” amesema Uwoya.
Akizungumzia suala la kudekezwa na kubembelezwa, Uwoya amesema yeye hajioni kuwa mtu anayependa kubembelezwa, bali anajitambua kama malkia na mtoto wa kwanza katika kundi hilo, hivyo anaamini anapaswa kusimama imara.
“Mimi si kwamba napenda kubembelezwa. Bila shaka mimi ni queen wa kweli, lakini mimi hata sidai kubembelezwa, maana kwenu mimi ni wa kwanza. Kwa hiyo mtoto wa kwanza lazima ukaze,” amesema.
Aidha, Uwoya ameeleza kuwa yeye ni mtu anayependa kusema ukweli bila kuzunguka, akisisitiza kuwa hapendi unafiki na kwamba wenzake ndani ya kundi hilo wanaifahamu tabia yake.
“Mimi ni mtu ambaye nimenyooka, sipendi kona kona. Kitu kama ni bluu nitasema bluu, siwezi kusema nyeupe,” amefafanua.
Ameongeza kuwa wakati mwingine hulazimika kujishusha ili kulinda umoja na kuendelea kuwa pamoja na wenzake, akiwataja Aunty, Wolper na yeye mwenyewe kuwa miongoni mwa wanaopenda kujishusha, huku akimtaja Kajala kuwa ndiye anayependa zaidi kudekezwa.
Kauli hiyo imeweka wazi namna mastaa hao wanavyoshughulikia tofauti zao na kudumisha urafiki wao licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza ndani ya kundi lao.




