Isarito: Nitafanya kazi na Mulky ila si kama zamani

MSANII wa filamu nchini, Isarito Mwakalindile, amesema hana tatizo kufanya kazi na msanii Mulky endapo watakutana kwenye mradi wa filamu, lakini amesisitiza kuwa ukaribu wao hautakuwa kama ilivyokuwa awali.
Isarito amefunguka hayo alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kufanya tena kazi na Mulky, ambaye awali walikuwa na ukaribu mzuri katika shughuli zao za sanaa.
Isarito amesema “Sina ugomvi na Mulky, lakini sitaki mazungumzo kuhusu uhusiano wa zamani yatafsiriwe tofauti na nilivyokusudia.
“Nikimaliza nimemaliza. Nimesema watu wengine tusiwaongelee. Sina tatizo naye, swali ulilouliza ni zuri, lakini mimi naweza kuliongelea vizuri halafu mtu akalipitisha kivingine.
“Kwenye kazi nitafanya naye, lakini nitaondoka haraka sana baada ya kazi kumalizika. Si kila kitu kinaweza kuwa kama mwanzo,” amrsema.
Aidha, Isarito ametoa msimamo wake kuhusu umuhimu wa kutenganisha mahusiano binafsi na ndoto za kazi, akisisitiza kuwa kuvunjika au kubadilika kwa mahusiano hakupaswi kuwa kikwazo cha maendeleo ya mtu.
“Ndiyo maana napenda kusema mapenzi yasizidi ndoto hata iweje. Kwenye ndoto yako, mimi nilikotoka nimeshakutana na watu wengi kabla ya hawa ninaoendelea kuachana nao. Sasa mtu mmoja afanye niharibu kazi, yeye nani?” amehoji.
Kauli hiyo inaweka wazi msimamo wa Isarito kuwa licha ya mabadiliko yanayoweza kutokea katika maisha binafsi, bado yuko tayari kushirikiana kikazi na watu aliowahi kuwa nao karibu, huku akisisitiza kuwa si lazima ukaribu wa zamani urejee.




