Kwingineko

Iran yalalamikia kunyanganywa tiketi za mashabiki kombe la dunia

NEW YORK: SHIRIKISHO la Soka la Iran (FFIRI) limelaani hatua ya kuondolewa kwa mgawo wa tiketi za mashabiki wake kuelekea Kombe la Dunia, siku chache kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa FFIRI, kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zinatoa asilimia nane ya tiketi za kila mchezo kwa nchi shiriki ili zigawiwe kwa mashabiki wake. Hata hivyo, Iran imedai kuwa imezuiwa kupata tiketi hizo licha ya baadhi ya mashabiki kuwa tayari wameshaanza maandalizi ya safari.

Katika taarifa yake, FFIRI ilisema hatua hiyo inakwenda kinyume na misingi ya usawa na haki katika mashindano ya kimataifa.

Iran inatarajiwa kucheza dhidi ya New Zealand Juni 15, Belgium Juni 21 na Misri Juni 26 katika hatua ya makundi ya mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Ushiriki wa Iran kwenye mashindano hayo umeendelea kugubikwa na changamoto mbalimbali zinazohusishwa na masuala ya kisiasa na usalama, ikiwemo vikwazo vya visa kwa baadhi ya maafisa wa timu hiyo.

Shirikisho hilo sasa limetaka FIFA kuingilia kati na kuhakikisha kanuni za usawa na kutobagua zinazingatiwa kwa nchi zote zinazoshiriki mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

Related Articles

Back to top button