Haaland akamia mataji

MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Erling Haaland amesema atafanya kila kitu kusaidia klabu hiyo kupata ubingwa wa kihistoria wa matatu mataji.
City imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Enngland msimu huu na inaweza kuongeza mataji mengine iwapo itazifunga Manchester United katika fainali ya Kombe la FA Juni 3 na Inter Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Juni 10.
Licha ya City kutawala mashindano ya ndani, haijawahi kubeba ndoo ya Ligi ya Mabingwa na Haaland ana matumaini anaweza kusaidia timu yake kufanikiwa kushinda michuano hiyo ya ngazi ya juu zaidi ya soka barani Ulaya.
“Itamaanisha kila kitu. Nitafanya kila niwezalo kujaribu kufanya malengo yatimie. Ni ndoto yangu kubwa na natumaini ndoto zitatimia,” amesema Haaland.
Mshambuliaji huyo amepata tuzo za mchezaji bora wa Ligi Kuu England na mchezaji bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo England(FWA).
Haaland amevunja rekodi ya Ligi Kuu England ya idadi ya mabao katika msimu mmoja na katika michuano yote kwa jumla katika msimu wake wa kwanza akiwa City akifunga mabao 52.