Kwingineko

GWIJI WA SOKA: Liverpool na England waomboleza Kifo cha Kevin Keegan

ENGLAND: Soka la dunia limepoteza mmoja wa mastaa wake wakubwa baada ya gwiji wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Kevin Keegan, kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Keegan, ambaye alijijengea jina kama mmoja wa washambuliaji bora wa kizazi chake, ameacha historia isiyofutika ndani na nje ya uwanja kutokana na mafanikio yake makubwa kama mchezaji na baadaye kocha.

Keegan aliiongoza Liverpool kutwaa mataji kadhaa ya Ligi Kuu ya England, Kombe la Ulaya pamoja na makombe mengine makubwa katika miaka ya 1970 kabla ya kuhamia Hamburg ya Ujerumani, ambako aliendelea kung’ara na kushinda tuzo mbili mfululizo za Ballon d’Or mwaka 1978 na 1979. Kwa England, aliichezea timu ya taifa mara 63 na kufunga mabao 21, akibaki kuwa mmoja wa wachezaji waliowahi kuheshimika zaidi nchini humo.

Baada ya kustaafu kucheza, Keegan aliingia kwenye ukocha na kuandika historia akiwa Newcastle United, alipoiongoza timu hiyo kupambana kwa karibu na Manchester United katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England katikati ya miaka ya 1990. Pia aliwahi kuinoa Manchester City na timu ya taifa ya England, huku akisifiwa kwa falsafa yake ya soka la kushambulia na kuwapa nafasi vipaji chipukizi.

Kifo vya Keegan kimezua majonzi makubwa katika ulimwengu wa soka, huku klabu ya Liverpool, Chama cha Soka cha England (FA), wachezaji wa zamani na mashabiki kutoka sehemu mbalimbali duniani wakitoa salamu za rambirambi. Wengi wamemtaja kuwa alikuwa zaidi ya mchezaji, bali kiongozi na mfano wa kujituma aliyehamasisha vizazi vingi vya wanasoka.

Urithi wa Kevin Keegan utaendelea kuishi kupitia mafanikio yake, heshima alizozipata na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya soka la England na dunia kwa ujumla. Atakumbukwa kama mmoja wa magwiji waliobadili historia ya mchezo huo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button