Feisal: Azam FC tumebadilika, tunaonesha hadhi ya klabu

DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Azam FC, Feisal Salum amesema wao kama wachezaji waliamua kujipanga upya baada ya mwenendo usioridhisha katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo ambalo sasa limeanza kuzaa matunda.
Feisal amesema hayo baada ya Azam FC kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KMC FC katika mchezo wa ligi uliochezwa jana, huku yeye akiibuka mchezaji bora wa mechi kutokana na kiwango kizuri alichoonesha.
“Mzunguko wa kwanza hatukuwa vizuri sana, tulipata sare 10, sio mwenendo mzuri. Lakini sisi kama wachezaji tumekaa na kuona raundi ya pili lazima tuoneshe kitu, tuoneshe utofauti ambao unaendana na hadhi ya klabu,” amesema Feisal.
Amesema ushindi huo ni matokeo ya mshikamano wa timu pamoja na kazi kubwa inayofanywa na benchi la ufundi na wachezaji wote.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tunaenda vizuri na sasa hivi tunaendelea vizuri,” amesema.
Kiungo huyo ameendelea kuwa kwenye kiwango bora katika michezo ya hivi karibuni, hali inayochangia mafanikio ya Azam FC katika mbio za kumaliza msimu kwenye nafasi nzuri.




