AFCONAfricaLigi KuuNyumbani

Kikosi bora cha Ligi Kuu Bara AFCON

LIGI Kuu Tanzania Bara imeendelea kuimarika kwa kushusha nyota wakubwa, ambao
wamekuwa wakiitwa kwenye timu za taifa na kuongeza chachu kwa vijana wa Kitanzania
kupambana.

Kitendo cha kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi 12 imeifanya Ligi Kuu Bara izidi kuimarika huku ikianza kufuatiliwa zaidi kutokana na ushiriki wa klabu zake
kwenye michuano ya Caf.

Yanga imekuwa timu ya kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na kupoteza kwa faida ya mabao ya ugenini.

Wakati Simba wao wakiwa ndani ya klabu 10 bora barani Afrika ikiwa imejikusanyia pointi 45 baada ya kucheza robo fainali nne za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la
Shirikisho.

Hivi sasa Ligi Kuu Bara inashika nafasi ya tano kwa ubora barani Afrika, hii inatokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika na kuongeza msisimko kwa washiriki.

Ubora wa Ligi Kuu Bara na kiwango kinachooneshwa na Simba na Yanga kimefanya Tanzania kupeleka timu nne kwenye mashindano ya Caf, mbili zikienda Ligi ya Mabingwa na mbili zikienda kushiriki Kombe la Shirikisho.

Ligi Kuu Bara ni miongoni mwa ligi ambazo zimetoa idadi kubwa ya wachezaji ambao ni 16
wanaoenda kushiriki fainali za mataifa ya Afrika nchini Ivory Coast ambazo zitaanza kutimua vumbi Januari 13.

HabariLEO linakuletea kikosi cha kwanza cha wachezaji wa mataifa mbalimbali wanaocheza katika Ligi Kuu Bara, ambao wataenda kuziwakilisha timu zao nchini Ivory Coast.

1.Djigui Diara -Yanga(Mali)
Kipa namba moja wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara ambaye ndiye anapewa nafasi kubwa ya kusimama kwenye milingoti mitatu ya timu ya taifa ya Mali.

Diara kwenye Ligi kuu Bara amekuwa na mwendelezo wa kiwango chake ambapo kwa misimu miwili amefanikiwa kuchukua tuzo ya kipa bora kwa misimu miwili mfululizo.

Lakini pia katika msimu wake wa pili akiwa na jezi ya Yanga aliisaidia timu hiyo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

2.Lusajo Mwaikenda-Azam (Tanzania)

Moja ya walinzi bora hivi sasa kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na vinara wa Ligi Kuu Bara, Azam FC, kiraka ambaye anacheza nafasi zote za eneo la ulinzi. Mlinzi huyu wa kulia
ambaye amekulia kwenye timu ya vijana ya Azam tangu akiwa kinda hivi sasa ni tegemeo kwenye jeshi la kocha Youssoupha Dabo.

3.Mohamed Hussein-Simba (Tanzania)
Miongoni mwa nyota wa kuigwa kwa vijana ni mlinzi huyu wa kushoto wa Simba ambaye ndiye mkongwe zaidi kwenye kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Licha ya panda shuka lakini Hussein ni miongoni mwa walinzi bora wa kushoto kwenye Ligi Kuu Bara ambaye msimu uliopita aliisaidia Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini pia alishika nafasi ya pili kwa kupiga pasi nyingi za mabao akipiga tano moja nyuma ya kinara Shomari Kapombe ambaye alipiga sita.

4.Ibrahim Bacca- Yanga (Tanzania)
Huyu ndio uti wa mgongo wa safu ya ulinzi ya Yanga ambaye katika misimu miwili iliyopita akiwa na jezi ya wananchi amefanikiwa kushinda makombe sita ya ligi za ndani. Bacca pia alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha Yanga fainali ya
Kombe la Shirikisho barani Afrika.

5.He- nock Inonga-Simba (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo)
Mlinzi wa kimataifa wa DRC ambaye ni mhimili kwenye safu ya ulinzi ya Simba ni miongoni mwa wachezaji ambao wamejihakikishia namba kwenye kikosi cha kocha Abdelhak
Benchikha.

Tangu ujio wake akitokea DRC amekuwa kwenye kiwango bora huku akishinda tuzo
ya beki bora msimu wa 2021/22. Lakini pia akiwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichocheza robo fainali mbili za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

6.Sospeter Bajana-Azam(Tanzania)
Kiungo wa ulinzi wa Azam ambaye amekuwa mhimili kwenye kikosi cha kocha Youssoupha Dabo, ambacho kiko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara. Nyota huyu ni zao la timu ya
vijana ya Azam ambaye hivi sasa amekuwa akiaminiwa mbele ya nyota kadhaa wa kigeni wanaocheza kwenye eneo la kiungo la Azam FC.

7.Kibu Denis -Simba (Tanzania)
Kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye tangu ametua kwenye kikosi hicho amekuwa kwenye kiwango bora na kuisaidia kucheza robo fainali mbili za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Nyota huyu ambaye anabebwa na kasi yake amekuwa miongoni mwa nyota waliojihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Benchikha.

8.Feisal Salum -Azam (Tanzania)
Moja ya talanta tuliyobarikiwa kuwa nayo ni kiungo huyu ambaye ni miongoni mwa usajili mpya kwenye kikosi cha Azam ambacho kipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Hadi sasa amechangia mabao 12 msimu huu akiwa amefunga mabao nane na kutoa pasi nne za mabao na kuisaidia timu yake kushika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

9.Kennedy Musonda -Yanga(Zambia)
Mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia na klabu ya Yanga ambaye amekuwa kwenye kiwango bora tangu alipotua hapa nchini akitokea Power Dynamos.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika huku hivi sasa akiwa amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Miguel Gamondi.

10.Clatous Chama-Simba (Zambia)
Moja ya viungo bora kuwahi kucheza kwenye Ligi Kuu Bara akiwa amecheza robo fainali tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na jezi ya Simba.

Chama ambaye mabao yake muhimu dhidi ya Nkana na AS Vita yameacha alama kwenye kikosi cha Simba na Ligi ya Mabingwa barani Afrika huku akiwa ni mchezaji mwenye rekodi ya kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja dhidi ya Horoya.

11.Stefan Aziz Ki-Yanga (Burkina Faso)
Kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara akiwa tayari amefunga mabao 10 na kutoa pasi mbili za mabao na kuwa na mwendelezo wa kiwango bora.

Huu ukiwa msimu wake wa tatu tayari ana medali sita za mataji ya ndani lakini pia akiwa na medali ya fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

 

Related Articles

Back to top button