Enzo hatiani kwa ubaguzi
Chelsea wameanza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya kiungo Enzo Fernandez baada ya kuweka video kwenye mtandao wa kijamii ambayo Shirikisho la Soka la Ufaransa lilisema ilijumuisha wimbo unaodaiwa kuwa wa “kibaguzi”.
Siku ya Jumanne FFF ilisema itawasilisha malalamiko kwa shirikisho la soka duniani Fifa, juu ya video hiyo iliyo na wimbo ulioimbwa na baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Argentina kuhusu wachezaji wa Ufaransa.
Mchezaji mwenzake wa Chelsea Fernandez Wesley Fofana, alichapisha picha ya video hiyo kwenye mtandao wa Instagram, akiielezea kama “ubaguzi wa rangi usiovumilika”.
Fernandez alisema “anasikitika sana” kwa video aliyochapishwa mtandaoni wakati Argentina ikisherehekea kushinda Copa America.
“Wimbo huo una maneno ya kukera sana na hakuna sababu kabisa ya maneno haya,” alisema.
“Ninapinga ubaguzi wa aina zote na ninaomba radhi kwa kutekwa na shangwe za sherehe zetu za Copa America.
“Video hiyo, nyakati hizo, maneno hayo, hayaakisi imani yangu au tabia yangu.”
Taarifa ya Chelsea ilisema: “Tunatambua na kuthamini msamaha wa mchezaji wetu na tutatumia hii kama fursa ya kuelimisha.
“Klabu imeanzisha utaratibu wa ndani wa kumpa adhabu.”
FFF itawasiliana na Chama cha Soka cha Argentina (AFA) kuhusu video ya moja kwa moja iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii na Fernandez baada ya Argentina kuifunga Colombia 1-0 kwenye fainali ya Copa America Jumapili.