Nyumbani

Edna Lema: Imekuwa ndoto kufundisha wanaume

KOCHA Mkuu wa Yanga Princess Edna Lema amesema ni kitu cha kujivunia kwake na anaona kama ndoto kupata nafasi ya kufanya kazi kwenye timu kubwa ya Yanga ya wanaume.

Kauli yake hiyo inakuja baada ya kujumuishwa kwenye kikosi hicho kwa mara ya kwanza ambapo atashiriki maandalizi ya mchezo dhidi ya Coastal Union.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Yanga Tv Dar es Salaam leo Edna amesema ni bahati kwake kwa kuwa anategemea kujifunza zaidi na kupata uzoefu kutoka kwa makocha wazoefu anaofanya nao kazi.

“Nawashukuru wote waliofanikisha wakiwemo Rais wa Yanga Hersi Said na viongozi mbalimbali. Kwangu mimi ni kitu kizuri kwangu, naenda kujifunza nia yangu ya kwenda pale ni kupata uzoefu,

“ Unaweza ukawa kocha mzuri lakini unahitaji uzoefu. Mpira siku zote ni kujifunza, mimi ni kocha mdogo ukilinganisha na viwango vya makocha wa Yanga ni vikubwa wamefundisha klabu kubwa mbalimbali,”amesema na kuongeza kuwa anamshukuru Kocha Mkuu Miloud Hamid ambaye amekuwa akimfuatilia na kumsapoti.

Kocha huyo mwenye leseni ya Diploma ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) amesema anaweza kupata muda sahihi wa kujifunza zaidi na kufika kule ambako anatamani kufika.

Kwa mujibu wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, Edna atamaliza muda wake na kikosi hicho baada ya mchezo dhidi ya Coastal Union.

Related Articles

Back to top button