COSOTA, TAA zaingia makubaliano kulipia mirabaha

DAR ES SALAAM: OFISI ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) zimeingia makubaliano kuhusu suala la kulipia leseni (mirabaha) kutokana na matumizi ya kazi za muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege.
Makubaliano hayo yalifanywa Dar es Salaam leo kati ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Cosota Doreen Sinare na Mkurugenzi Mkuu wa TAA Abdul Mombokaleo na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ‘Mwanafa’ na Naibu Waziri Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile.
Akizungumza kwenye hafla hiyo ya utiani saini Mwinjuma amesema makubaliano hayo ni jitihada za Dk Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha sekta ya sanaa na muziki katika nchi inachagiza maendeleo ya wasanii na kuleta tija.
Amesema makubaliano hayo yatasaidia kuhakikisha wasanii wa muziki wanapata haki yao ya malipo kutokana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege nchini.
“Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kusisitiza wasanii wanatakiwa kunufaika na kazi zao kwani muziki wa Tanzania unasikika katika maeneo ya umma kama vile viwanja vya ndege, na hivyo kuonesha talanta za wasanii na pia kutoa fursa za kibiashara.
Amesema kwa mujibu wa makubaliano hayo, TAA itahakikisha kuwa inazingatia masharti ya kulipia mirabaha inayohusiana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege na kwa upande mwingine kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya nyimbo zinazopigwa ni za Tanzania na asilimia 20 ndio za nje ya Tanzania.
Amesema makubaliano hayo yanalenga kutoa fursa kwa wasanii kupata malipo stahiki kutokana na matumizi ya kazi zao. Pia, yatasaidia kuleta uwazi katika michakato ya ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha, huku ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuendeleza na kulinda sekta ya sanaa na burudani nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile ameipongeza Cosota na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa kubuni na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa agizo la Rais juu ya kubuni njia za ziada za kukuza kipato cha wasanii na Taifa.
Ametoa wito kwa taasisi zingine chini ya Wizara ya Uchukuzi, hususani Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na TASHICO kuwasiliana na COSOTA na kuiga mfano mzuri uliowekwa na TAA.
“Ni imani yangu, kupitia taasisi zetu, Wizara ya Uchukuzi itakuwa imechangia ipasavyo katika kutekeleza agizo la Rais, na mwisho wa siku kuwafaidisha ipasavyo wasanii wetu wa muziki kupitia kazi zao,”amesema na kuahidi kuwa watahakikisha asilimia themanini (80) ya nyimbo zinazopigwa ni za Tanzania kama ilivyoelekezwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Cosota Doreen Sinare amesema wasanii wajisajili na kuwa rasmi na kutengeneza kazi zenye ubora ili zipate nafasi ya kupigwa na kutumika katika maeneo mbalimbali.