Comnet Zanzibar ndiyo mabingwa resi za Ngalawa 2026

ZANZIBAR:KAMPUNI ya Comnet Zanzibar imeibuka mabingwa wa mashindano ya resi za ngalawa yaliyofanyika katika ufukwe wa Serena, Unguja, Juni 28, 2026, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuhitimisha Tamasha la 29 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF).
Mashindano hayo yalishirikisha ngalawa 11 kutoka taasisi na kampuni mbalimbali, ambapo Comnet iliongoza mbio hizo na kutwaa nafasi ya kwanza baada ya kuwashinda washiriki wengine 10 waliokuwa wakiwania ubingwa wa mwaka huu.
Akizungumza baada ya mashindano hayo, Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale, aliwatangaza washindi, akisema nafasi ya pili ilichukuliwa na Azam Media, nafasi ya tatu ikakwenda kwa ZIFF, huku Robin Batista akimaliza katika nafasi ya nne.
Washiriki wengine waliojumuika katika mashindano hayo ni pamoja na Zanzibar Marine Association (ZMA), Fish Market, WIOMSA, UN Women na taasisi nyingine zilizoshiriki kuonesha ushindani na kuunga mkono tamasha hilo.
Katika hafla hiyo, Mjumbe wa Bodi ya ZIFF, Profesa Martin Mhando, aliwapongeza washindi na kukabidhi zawadi, akieleza kuwa mashindano ya ngalawa ni sehemu muhimu ya kuenzi urithi wa bahari na utamaduni wa Waswahili wa mwambao.
Mashindano hayo yaliandaliwa kupitia jukwaa la Women Panorama kwa lengo la kuendeleza mchezo wa jadi wa ngalawa, kuutangaza kama kivutio cha utalii na kuunganisha sanaa, michezo na utamaduni katika Tamasha la ZIFF.
Resi za ngalawa zimeendelea kuwa moja ya matukio yanayovutia maelfu ya watazamaji wakati wa ZIFF, zikitoa burudani na kuonyesha historia, ustadi na utamaduni wa Zanzibar kupitia urithi wa bahari.




