Chama: Haikuwa rahisi ila tumetoboa

DAR ES SALAAM: KIUNGO mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya JKT Tanzania jana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo haukuwa rahisi kutokana na ugumu wa mchezo huo hasa kipindi cha kwanza.
Chama ambaye ndiye aliyefunga bao pekee la ushindi, amesema walitarajia kupata bao la mapema ili kuwasaidia kuutawala mchezo kutokana na uchovu wa ratiba ya mechi nyingi.
“Mchezo haukuwa mzuri sana kwetu, kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu. Tulitegemea tunaweza kupata bao mapema ili tumiliki mchezo kwa sababu tulitoka kucheza Jumapili, hivyo tuliamini tukipata goli mapema lingetupa nguvu zaidi,” amesema Chama.
Amesema baada ya kumaliza dakika 45 za kwanza bila kufunga, walilazimika kuongeza nguvu kipindi cha pili kufuatia maelekezo ya benchi la ufundi.
“Tulienda mapumziko bila kupata bao, hivyo kocha alituambia tupambane zaidi ili tuweze kupata goli la ushindi,” amesema.
Mbali na kuifungia Simba bao la ushindi, Chama pia ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi na kusema mafanikio hayo yametokana na juhudi za timu nzima.
“Tuzo niliyopata ni kwa ajili ya timu kwa sababu wote tunapambana kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Chama.




