
ZANZIBAR: KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kulingana na ubora wa kikosi chake anaimani hakuna timu ambayo itamsumbua katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Gamond amesema kwasasa wamewaacha mbali wapinzani wao, huku akiwataka wadau kuiheshimu klabu hiyo na kutoiweka daraja moja na timu nyingine kwa sababu ya ubora wa wachezaji aliokuwa nao.
Kauli ya Gamondi ni kama amemjia juu Kocha wa Singida Black Stars, Patrick Aussems aliyesema Yanga ni ya kawaida kabla ya mchezo wa jana usiku kisha akaambulia kipingo cha bao 1-0 dhidi ya vinara hao wa ligi kuu katika mchezo uliopigwa visiwani Zanzibar.
“Yanga tuko daraja lingine,kuna muda tunavunjiwa sana heshima huwezi kuja kucheza na sisi ukaja kutulinganiusha na Pamba au timu nyingine kuna muda inabidi kumuheshimu mpinzani.
Nilitarajia hili kuwa mchezo utakuwa mgumu sana ila sisi tumetengeneza nafasi zaidi yao, wao walikuwa wanacheza mipira ya juu pekee,nimefurahi kwa kiwango bora cha wachezaji wangu wamecheza vizuri sana,” amesema Gamondi.