Simba haiwachukulii poa B19

DAR ES SALAAM : WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamesema sare waliyopata kwenye dabi dhidi ya Yanga umeipa timu hiyo kujiamini na kurejesha heshima, huku akisisitiza kuwa sasa nguvu zao zinaelekezwa katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya timu ya Championship B19.
Akizungumzia mchezo huo Dar es Salaam leo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally amesema mchezo huo utakaochezwa jumamosi katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, hawauchukulii kirahisi licha ya B19 kuwa timu ya daraja la chini, kwani Simba ina malengo makubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo msimu huu.
“Simba mpya imezaliwa pale Zanzibar. Nguvu kubwa tunaielekeza kwenye mechi dhidi ya B19. Ni timu ya daraja la chini lakini hatuichukulii kawaida wala poa, tunaitazama kama mpinzani tishio kwa sababu kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB tuna malengo ya kuchukua kombe,” amesema Ahmed.
Amesema kuwa timu imeanza maandalizi ya mchezo huo huku tiketi tayari zikiwa zimeanza kuuzwa, akiwahimiza mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu yao.
“Nawaomba Wanasimba, najua bado tuna furaha kubwa ya kiwango kilichooneshwa na timu katika mchezo uliopita, lakini sasa tuelekeze nguvu zetu kwenye mchezo ujao,
‘’ Kila kitu tulichokitumia kwenye dabi tutakitumia pia dhidi ya B19 na kwenye michezo mingine kwa sababu tunahitaji ubingwa msimu huu,” amesema.
Mwisho




