Kwingineko

Bosi West Ham aachia ngazi

LONDON, England: MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya West Ham United, Karren Brady, amejiuzulu rasmi nafasi yake baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka 16, hatua iliyotangazwa Jumanne na klabu hiyo ya Ligi Kuu England.

Brady ameondoka katika kipindi ambacho West Ham inapitia changamoto za matokeo uwanjani, ikiwa kwenye vita ya kushuka daraja, huku ikishika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Katika taarifa yake, Brady amesema amekuwa na heshima kubwa kufanya kazi na bodi ya klabu, wachezaji, wafanyakazi na mashabiki kwa muda wote aliokuwa klabuni hapo.

“Imekuwa heshima kubwa kufanya kazi na bodi, uongozi, wachezaji, wafanyakazi na mashabiki wa West Ham United. Pamoja tumefanikisha mafanikio makubwa, lakini kwangu kumbukumbu kubwa itabaki kuwa kushinda kombe la UEFA Europa Conference League,” amesema Brady.

Mafanikio hayo aliyoyataja ni ushindi wa West Ham katika michuano ya UEFA Europa Conference League Final 2023, ambayo ilibaki kama moja ya matukio makubwa katika historia ya klabu hiyo.

Brady alikuwa miongoni mwa viongozi walioshiriki mabadiliko makubwa ya klabu, ikiwemo uhamisho kutoka uwanja wa Upton Park hadi London Stadium mwaka 2016, hatua iliyoongeza uwezo wa mashabiki kufikia takribani viti 60,000.

Hata hivyo, kipindi chake kilikumbwa pia na changamoto na malalamiko ya mashabiki kuhusu ongezeko la bei za tiketi na mwenendo wa klabu, hali iliyomfanya kuwa mtu mwenye maoni mchanganyiko miongoni mwa wapenzi wa timu hiyo.

Kwa sasa West Ham inaendelea kupambana kujinusuru kushuka daraja katika msimu unaoendelea wa Premier League.

Related Articles

Back to top button