
LONDON, England
BINGWA mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain (PSG) wameonesha ubora wao kwa kuichapa Chelsea mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo katika Uwanja wa Stamford Bridge.
Ushindi huo umeifanya PSG kusonga mbele kwa jumla ya mabao 8-2, ikiwa ni moja ya vipigo vizito kuwahi kuipata Chelsea katika mashindano ya Ulaya.
PSG ilianza mchezo huo kwa kasi, ikipata bao la mapema dakika ya sita kupitia Khvicha Kvaratskhelia kabla ya Bradley Barcola kuongeza la pili dakika ya 14, mabao hayo ya mapema yalizima matumaini ya wenyeji kurejea mchezoni.
Chelsea walijaribu kusaka mabao kupitia Cole Palmer, Enzo Fernandez na Pedro Neto lakini walishindwa kutumia nafasi walizozipata, huku PSG wakionekana kuwa hatari zaidi kwenye mashambulizi ya kushtukiza.
Bao la tatu lilifungwa na kinda Senny Mayulu aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa, akihitimisha karamu ya mabao kwa upande wa wageni.
Mashabiki wa Chelsea walionekana kukerwa na matokeo hayo, wakionesha wazi kutoridhishwa kwao, huku baadhi yao wakimtaja mmiliki wa zamani Roman Abramovich na kuukosoa uongozi wa sasa wa klabu hiyo.
Akizungumza baada ya mchezo, Kocha Mkuu wa Chelsea, Liam Rosenior, amesema: “Hii ni klabu kubwa yenye mashabiki wanaohitaji mafanikio ya haraka. Naelewa kabisa hisia zao, nasi tunahitaji kubadilika ili kuwapa wanachotarajia.”
Katika pigo jingine, Chelsea walimpoteza beki wao Trevoh Chalobah aliyepata majeraha ya kifundo cha mguu, hali inayoweza kuathiri kikosi hicho katika mbio za kuwania kumaliza msimu kwenye nafasi nne za juu Ligi Kuu ya England.




