Bellingham:Nipo tayari kubadilika
‘MIDO’ ya mpira kutoka Real Madrid Jude Bellingham amesema anafurahia zaidi kucheza katika nafasi ya mshambuliaji lakini yuko tayari kubadilika kuhakikisha anaingia katika mfumo mpya wa Mwalimu wa Los Blancos Carlo Ancelotti ili aweze kuisaidia timu hiyo kupata matokeo.
Bellingham ambaye amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Real Madrid ameisaidia timu hiyo kushinda taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu uliopita, lakini hajawa na msimu mzuri baada ya kuhamishiwa katika nafasi ambayo hahusiki moja kwa moja na ushambulizi kufuatia kuwasili kwa mshambuliaji Mfaransa Kylian Mbappe kutoka PSG.
Kiungo huyo mwenye miaka 21 alianza vyema msimu uliopita akifunga mabao 8 katika mechi 9 za Laliga lakini ana mabao mawili pekee msimu huu.
“Inabadilisha ‘story’ kidogo, mtindo wa uchezaji na mbinu, lakini nimeonesha kuwa naweza kucheza katika nafasi tofauti. Napendelea zaidi mbele, lakini sio muhimu kwangu.”
“Nipo tayari kucheza popote watakaponiweka na siathiriwi na nafasi hiyo, huwa tunapanga timu ili kushinda…nilikuja hapa msimu uliopita na klabu ikampoteza Benzema, mmoja wa wachezaji bora kwangu”
“Kulikuwa na pengo na ilikuwa ni moja ya njia za kuziba, mwaka huu tuna mchezaji bora zaidi kutokea wa kizazi hiki, amefunga magoli mengi sana. Nafasi yangu itabadilika na niko tayari kwa hilo” – Amesema Bellingham
Real Madrid watakuwa kibaruani leo Novemba 27 dhidi ya Liverpool dimbani Anfield majira ya saa 5 usiku kabla ya kuwakabili Getafe kwenye La Liga Jumapili.