BASATA yajadili kutangaza sanaa za Tanzania kupitia Miss World 2026

DAR ES SALAAM: BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limeanza maandalizi ya kuitangaza Tanzania kupitia sanaa na ubunifu katika mashindano ya Miss World 2026, yatakayofanyika nchini Vietnam.
Hatua hiyo imejiri baada ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi wa BASATA, Bona Masenge, kufanya mazungumzo na Miss World Tanzania 2026, Latricia Ian, pamoja na waratibu wa Miss World Tanzania katika ofisi za BASATA zilizopo Kivukoni, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zilijadili mapendekezo ya aina ya zawadi ya kisanaa itakayowakilisha Tanzania katika mnada maalumu utakaofanyika sambamba na mashindano ya Miss World 2026.
“Lengo la zawadi hiyo ni kuonesha ubunifu wa wasanii wa Tanzania huku ikitangaza utamaduni, urithi na utambulisho wa taifa mbele ya washiriki na wadau mbalimbali kutoka duniani kote.”amesema Bona
BASATA imeeleza kuwa ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo la kimataifa ni fursa muhimu ya kuitangaza sekta ya sanaa za ubunifu, kuhamasisha thamani ya kazi za wasanii wa ndani na kuongeza mwonekano wa urithi wa kitamaduni wa Tanzania katika soko la kimataifa.
Kupitia ushirikiano huo, Baraza linaendelea kuhimiza matumizi ya sanaa kama nyenzo ya diplomasia ya utamaduni na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia kazi zenye ubunifu na zinazobeba utambulisho wa taifa.




