Nyumbani

Wiki ya Simba kuzinduliwa Kreta ya Ngorongoro

ARUSHA: Klabu ya Simba imechagua eneo la kipekee la Kreta ya Ngorongoro kuzindulia rasmi maadhimisho ya Wiki ya Simba mwaka huu, huku viongozi wakieleza kuwa tukio hilo linalenga kuunganisha michezo na utalii.

Akizungumzia kuhusu maandalizi hayo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally amesema uzinduzi utafanyika Julai 25 katika eneo la Hippo Pool (Ngoriktoktok) lililopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo watashuka ndani ya kreta kushiriki tukio hilo la kihistoria.

Amesema uzinduzi wa Wiki ya Simba umekuwa ukifanyika katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Morogoro na Mafinga, lakini safari hii wameamua kuhamishia tukio hilo ndani ya moja ya vivutio vikubwa vya utalii duniani ili kuongeza mvuto na kuitangaza Tanzania.

“Kila anayesikia Ngorongoro au kreta hupata hamu ya kufika. Tumeona ni sehemu sahihi kuipa Wiki ya Simba hadhi ya kipekee huku tukichangia kutangaza utalii wa nchi yetu,” amesema.

Aidha, amewaalika mashabiki wote wa Simba kushiriki uzinduzi huo, akieleza kuwa gharama za kushuka ndani ya kreta zitagharamiwa na Klabu ya Simba kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Kwa mujibu wa ratiba, msafara wa Simba utaondoka Dar es Salaam kuelekea Arusha kabla ya kulala Karatu, kisha asubuhi yake kuelekea Ngorongoro kwa shughuli za uzinduzi zitakazojumuisha hotuba za viongozi, burudani na shughuli mbalimbali za kuashiria kuanza rasmi kwa Wiki ya Simba.

Baada ya uzinduzi huo, kutakuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali yatakayofanyika katika kipindi chote cha Wiki ya Simba.

Related Articles

Back to top button