Ligi Kuu

Kamwe: Mechi tano zilizobaki ni fainali

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe, amesema mechi tano zilizobaki kwa timu hiyo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni sawa na dabi kutokana na ushindani mkubwa uliopo.

Yanga imetoka kushinda mchezo wake uliopita dhidi ya Namungo mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam jana.

Kamwe amesema katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu, kila mchezo una umuhimu mkubwa hivyo wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wanapaswa kuongeza jitihada ili kuhakikisha timu inafikia malengo yake.

“Mechi tano zilizobaki zote ni dabi. Kila mechi tuweke jitihada kwa sababu mazingira ni magumu, mashabiki huu muda ni kujitoa,” amesema Kamwe.

Amesema kwa sasa kipaumbele kikubwa kwa Yanga ni kuhakikisha wanashinda michezo iliyosalia badala ya kujikita katika maneno au presha kutoka kwa wapinzani wao.

“Wanayanga kipaumbele chetu iwe ni mechi zilizobaki, tuachane na maneno ya wapinzani,” amesema.

Kauli hiyo inakuja wakati mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu zikizidi kushika kasi huku kila timu ikipambana kukusanya pointi muhimu katika hatua za mwisho za msimu.

Related Articles

Back to top button