Simba yang’aa kwa Pamba jiji CCM Kirumba
MWANZA: WEKUNDU wa Msimbazi Simba imeibuka na ushindi 1-0 Dhidi ya Pamba Jiji FC, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara jioni ya leo uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Bao la Simba limefungwa na Leonel Ateba kwa penalti dakika ya 22 baada ya kufanyiwa madhambi na nahodha wa Pamba Jiji Christopher Okoje.
Kwa ushindi huo, Simba inayonolewa na Kocha Fadlu Davids inafikisha pointi 28 na kuendelea kuongoza ligi mbele ya watani wao Yanga walio nafasi ya pili tofauti ya alama nne na mchezo mmoja mkononi.
Licha ya kuwa na mambo mengi ambayo yalikuwa yanaendelea tangu jana jijini Mwanza, lakini Simba wameonyesha ukubwa mbele ya Pamba Jiji FC .
Simba ni mchezo wa tano wanaocheza ugenini na kushinda mechi zote huku akipoteza mechi moja nyumbani dhidi ya Yanga na sare na Coastal Union.
Kikosi cha Simba kinarejea jijini Dar es Salaam leo, wakitokea Mwanza na kuingia kambini moja kwa moja kujiandaa na mchezo wa hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola unaotarajiwa kucheza Jumatano, Novemba 27, uwanja wa Benjamin Mkapa.