Arajiga ataamua Dabi Jumamosi

DAR ES SALAAM: ZIKIWA zimebaki siku tatu pekee kuelekea mchezo mkubwa wa Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba, Bodi ya Ligi Tanzania imemtangaza Ahmed Arajiga kutoka Manyara kuwa mwamuzi wa mchezo huo utakaochezwa Machi 8.
Arajiga atasaidiwa na Mohammed Mkono kutoka Tanga pamoja na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam, huku Amina Kyando akiwa mwamuzi wa akiba katika pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.
Mwamuzi huyu ana historia ya kuchezesha mechi za Dabi ya Kariakoo, akihusika katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa msimu uliopita ambapo Yanga iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Simba.
Hii itakuwa mara yake ya nne kusimamia mchezo wa Dabi ya Kariakoo. Katika mara tatu zilizopita, Yanga imeshinda michezo miwili, huku Simba ikipata ushindi mara moja.
Rekodi zake zinaonesha kuwa Julai 2021, alichezesha fainali ya Ngao ya Jamii ambapo Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Yanga. Mei 2022, Arajiga alisimamia nusu fainali ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga ilishinda kwa bao 1-0.
Ushindi wake mkubwa zaidi ulirekodiwa Novemba 2023, ambapo Yanga iliichabanga Simba mabao 5-1 katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa rekodi hizi, macho yote yatakuwa kwa Arajiga kuona jinsi atakavyosimamia mchezo huu mkubwa, huku mashabiki wakitarajia mwamuzi mwenye haki na usawa kwa pande zote mbili.