La Liga

Raphinha mbioni kurejea mazoezini wiki hii

BARCELONA, Hispania: KLABU ya Barcelona imepata ahueni kubwa baada ya kurejea kwa wachezaji wawili muhimu wakati ikikaribia kutwaa ubingwa wa La Liga msimu huu.

Taarifa zinaeleza kuwa nyota Raphael Belloli ‘Raphinha’ pamoja na kiungo chipukizi Marc Bernal wanatarajiwa kurejea mazoezini wiki hii, jambo linaloongeza nguvu kikosini mwa kocha Hansi Flick kuelekea mechi muhimu dhidi ya Osasuna.

Barcelona ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa mapema mwishoni mwa wiki ijayo, iwapo itashinda mchezo wake huo ujao na wakati huo huo, Real Madrid ikishindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Espanyol.

Hata hivyo, safari ya kwenda Pamplona si rahisi kwa Barcelona, hasa ikizingatiwa kuwa msimu uliopita ilipoteza kwa mabao 4-2 kwenye uwanja huo.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa kinda Lamine Yamal ambaye ameumia misuli ya paja na atakosekana hadi mwisho wa msimu.

Kurejea kwa Raphinha kunatajwa kuwa na umuhimu mkubwa zaidi, hasa kutokana na pengo lililoachwa na Yamal. Mshambuliaji huyo wa Brazil anaweza kuimarisha safu ya ushambuliaji, iwe upande wa kulia au kushoto ambapo kwa sasa Marcus Rashford na Fermín López wamekuwa wakicheza kwa muda.

Kwa upande wa Bernal, ushindani ndani ya kikosi ni mkubwa baada ya kurejea kwa Frenkie de Jong na kiwango kizuri cha Gavi, hali inayomaanisha atalazimika kupambana ili kurejesha nafasi yake ya kwanza.

Iwapo wachezaji hao watarejea kwa wakati na kuwa fiti, Barcelona itakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kumaliza kazi na kutwaa ubingwa wa La Liga mapema kabla ya mwisho wa msimu.

Related Articles

Back to top button