Kwingineko

Lingard aandika historia Brazil

Amtaja Neymar kuwa kipimo kikubwa

BRASILIA, Brazil: KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Jesse Lingard, ameendelea kuandika historia baada ya kuwa Muingereza wa kwanza kucheza katika ligi kuu ya Brazil akikitumikia klabu ya Corinthians.

Lingard (33) ambaye alijiunga na Corinthians akitokea FC Seoul, amesema anafurahia changamoto mpya huku akilenga kushinda mataji akiwa Brazil. Tayari amefunga bao lake la kwanza katika michuano ya Copa do Brasil, hatua inayodhihirisha kuanza vizuri katika maisha yake mapya ya soka.

Akizungumza na BBC, Lingard amesema licha ya wengi kushangazwa na uamuzi wake kuhamia Brazil, bado anaamini ana uwezo wa kucheza katika kiwango cha juu. “Nilikuwa na ofa nyingi mezani, lakini nilihitaji kujipima zaidi na kupata changamoto mpya,” amesema.

Ameeleza kuwa maisha ya Brazil ni tofauti, hasa kutokana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa Corinthians ambao wamekuwa wakifika hata uwanjani kushuhudia mazoezi ya timu yao. Aidha, lugha imekuwa changamoto kwake, lakini ameanza kujifunza Kireno ili kurahisisha mawasiliano.

Kuhusu maisha yake ya zamani, Lingard amekiri kuwa alikuwa na kipindi kizuri ndani ya Manchester United, lakini alihitaji mabadiliko ili kujipa nafasi ya kuanza upya, akianza safari yake Asia kabla ya kutua Brazil.

Pia amepongeza maendeleo ya United chini ya kocha Michael Carrick, akisema timu hiyo ipo kwenye mwelekeo sahihi na anastahili kupewa nafasi ya kudumu. Aidha, amemsifia nahodha Bruno Fernandes kwa kiwango chake bora msimu huu, akiamini anastahili kuwania tuzo ya mchezaji bora duniani.

Akizungumzia changamoto ya kukutana na nyota wa Brazil, Lingard amemtaja Neymar kuwa miongoni mwa wachezaji anaowaheshimu na angependa kucheza dhidi yake ili kujipima zaidi.

Kwa upande wa Kombe la Dunia 2026, Lingard ameziweka England national football team, Brazil na Ufaransa kama timu zenye nafasi kubwa ya kufanya vizuri, huku akiamini England inaweza kutwaa ubingwa ikiwa itaendelea na kiwango hicho.

 

Related Articles

Back to top button