Cole aipa silaha Chelsea kuiua Man City

LONDON, England: KIUNGO wa zamani wa Chelsea, Joe Cole, amesema hofu ya kukutana na Manchester City inaweza kuisaidia timu hiyo kutoa kiwango bora katika fainali ya FA Cup mwezi ujao.
Chelsea imefanikiwa kutinga fainali baada ya kuifunga Leeds United kwa bao 1-0 kwenye dimba la Wembley Stadium, bao lililofungwa na Enzo Fernández katika kipindi cha kwanza.
Ushindi huo umeipa Chelsea nafasi ya kukutana na mabingwa watetezi Manchester City, timu ambayo Cole ameielezea kama “mbwa mwitu wakubwa” kwa ubora wao wa sasa chini ya kocha Pep Guardiola.
Cole amesema licha ya ubora wa City, Chelsea ina uwezo wa kushinda mechi kubwa, akisisitiza kuwa baadhi ya wachezaji hutoa kiwango cha juu wanapokuwa na presha au hofu.
“Manchester City ndiyo timu ya kuifunga kwa sasa, lakini Chelsea imekuwa ikipeleka ushindani mkubwa kwenye mechi kubwa.
Wakati mwingine hofu huwafanya wachezaji kucheza kwa kiwango cha juu zaidi,” amesema Cole.
Kwa upande wake, kocha wa muda Calum McFarlane amepongeza ari ya wachezaji wake, akimtaja Fernández kama mpiganaji aliyebadili mwelekeo wa mchezo.
Chelsea ina nafasi ndogo ya kumaliza katika nafasi za juu za Premier League ili kufuzu UEFA Champions League, hivyo fainali hiyo inabeba matumaini makubwa ya kumaliza msimu kwa mafanikio.
Hata hivyo, rekodi inaonesha Chelsea haijaifunga Manchester City tangu walipokutana kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2021, jambo linaloifanya kuingia fainali hiyo kama timu isiyopewa nafasi kubwa.




