Chuji avutiwa kiwango Cha Abuya

DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa zamani wa Simba na Yanga , Athuman Idd ‘Chuji’, amempongeza kiungo wa Yanga Duke Abuya, kufuatia kiwango bora alichoonesha msimu huu.
Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii, Chuji ameandika maneno mafupi lakini yenye uzito mkubwa akisema: “Nakupa heshima ya juu 2024/2025”, akionesha kuvutiwa na mchango wa Abuya katika michuano hiyo.

Katika mchezo dhidi ya Azam FC juzi ambayo Yanga ilishinda mabao 2-1 Abuya aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.
Abuya ameonekana kuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia macho kutokana na uchezaji wake imara wa kiungo, akichangia timu yake kufanya vizuri katika mashindano ya Muungano Cup na hata Ligi Kuu.
Chuji ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri miaka ya nyuma akizitumikia Simba na Yanga kwa nyakati tofauti kutokana na kiwango bora. Pia, aliwahi kuzitumikia timu za taifa kuanzia ngazi ya vijana hadi taifa Stars.
Michuano ya Muungano Cup imeendelea kuvutia watazamaji kutokana na ushindani mkali kati ya timu mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar, huku wachezaji wakipata nafasi ya kuonesha vipaji vyao.




