Amorim: Simchukii Rashford

BUCHAREST:Kocha mkuu wa mashetani wekundu Manchester United Ruben Amorim amesema hana chuki binafsi na mshambuliaji wake Marcus Rashford bali kuna changamoto za kinidhamu za mchezaji huyo ambazo anapaswa kuzirekebisha kabla ya kujumuishwa tena kikosini.
Amorim ameyasema hayo akijibu swali la mwandishi wa habari katika mkutano na waandishi hao kuelekea mechi yao ya Europa League dhidi ya FCSB ya Romania ambapo mwandishi mmoja alitaka kujua ni kwanini kocha Amorim amekuwa hamjumuishi Rashford kikosini mara kwa mara.
“Em fikiria kuwa na mtu kama Rashford, timu yetu inapaswa kuwa bora zaidi akiwepo, lakini huyu Rashford ni lazima abadilike akibadilika tutamkaribisha tena kikosini kwa sababu tunamhitaji. Lakini kwa sasa iwe wazi kwamba kuna mambo tunayataka kwake na yeye akiwa tayari tunamsubiri” – Amesema kocha Amorim
Kwa upande mwingine Amorim ameonesha kukerwa na watu ambao wanataka kufanya suala hilo lionekane kama anamchukia Rashford na ndio maana hamjumuishi kwenye kikosi chake.
“Unajua mnataka kufanya suala hili kama chuki binafsi, mimi simchukii Marcus hata kidogo ninajaribu tu kuweka sheria moja kwa kila mtu na kwa kwangu ni rahisi tu kitu kimoja kwa kila mtu” ameongeza
Marcus Rashford amekuwa na wakati mgumu tangu kuwasili kwa kocha huyo Mreno aliyekamatilia timu hiyo tangu Novemba mwaka jana, akicheza mechi 3 akifunga mabao 3 akiwa na wastani mzuri wa bao kwenye kila mechi.