Al Hilal wamfungia kazi Salah

RIYADH:MABINGWA wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia ‘Saudi Pro League’ Al Hilal wako tayari kumpa mkataba mnono winga wa Liverpool Mohammed Salah iwapo atachagua kuikacha Ulaya na kwenda kuishi nchini Saudia ikiwa ni harakati za klabu hiyo kuziba pengo la Mbrazil Neymar Jr.
Mkataba wa Neymar unamalizika mwishoni mwa msimu huu na Al Hilal wanaona winga huyo wa Liverpool ni chaguo sahihi kwa nafasi hiyo. Kwa mujibu wa Sky Sports Salah hana mpango wa kwenda Saudi Arabia kwa sasa na anaamini bado ana nafasi katika soka la ushindani barani Ulaya.
Salah mwenye miaka 32 anamaliza mkataba wake na Liverpool mwishoni mwa msimu huu na amekuwa huru kuzungumza na timu yeyote tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Taarifa za Salah kutimkia Saudi Arabia zimezuka tena baada ya mmoja ya watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa zaidi kwenye soka la nchi hiyo ya kiarabu Turki Alalshikh kuposti picha ya Salah akiwa na uzi wa Al Hilal hapo jana
Mwezi Agosti Mwaka 2023, Liverpool ilikataa dau la zaidi ya Pauni milioni 150 kutoka kwa Al Ittihad waliotaka saini ya winga huyo raia wa Egypt na swali linabaki kuwa je Salah atavutiwa na pesa za Waarabu?