Akothee aeleza alichokutana nacho nje ya uhusiano na meneja wake

NAIROBI: MWIMBAJI Esther Akoth maarufu Akothee ameandika ujumbe mzito wa siku ya kuzaliwa kwa mpenzi wake Nelly Oaks ambaye pia ni meneja wake akielezea changamoto kadhaa walizopitia katika uhusiano wao.
Katika chapisho lake la mtandao wa kijamii, Akothee alifunguka kuhusu vikwazo walivyokumbana navyo wakiwa pamoja huku akiweka wazi jambo kubwa la kusaka mapenzi nje ya mapenzi yao ambapo mara kwa mara walijaribu kuachana lakini baada ya muda walirudiana.
“Tumejaribu kuachana, tukajaribu kwingine lakini sote tulikosa amani huko nje tukajikuta tunarudi. Hatujui jinsi ya kuachana. Tunachojua ni jinsi ya kurudi na kuwa pamoja.” Aliandika Akothee mwanamuziki mwenye vituko vingi.
Akothee akuacha kumsifia Nelly Oaks, ambaye pia ni meneja wake, akitoa shukrani zake kuu: “Leo, katika siku hii maalum, ninataka kutoa shukrani zangu za dhati kwa wazazi wako kwa kuleta jiwe la thamani kama hili ulimwenguni. Safari yetu ya pamoja, iliyojaa misukosuko, inathibitisha uimara wa uhusiano wetu.”
Akothee alisisitiza mchanganyiko wa kipekee wa biashara na maisha ya kibinafsi wanayoshiriki, akibainisha jukumu muhimu la Nelly Oaks katika mafanikio yake ya kitaaluma. “Ninatabasamu hadi kwenye benki na Brand Akothee kwa sababu yako. Wakati wowote kampuni inalipa, au mkataba mpya unapotiwa saini, wewe ndiye mtu wa kwanza ninayekupigia simu kushiriki furaha yangu na huwa unajivunia mimi.”