
DAR ES SALAAM: Rapa kutoka Marekani, Cardi B, amesema hana mpango wa kuendelea kuwa single maisha yake yote, akisisitiza kuwa licha ya kufurahia maisha yake binafsi, bado anatamani kuwa na mpenzi.
Akijibu mashabiki waliomtaka aendelee kuwa single na kujikita katika maendeleo yake binafsi, Cardi amesema hana sababu ya kubaki bila mwenza milele.
Akizungumza kwenye mtandao wa X, Cardi ameeleza kuwa amekuwa single kwa kipindi chote cha ziara yake ya muziki na hakuwahi kuzungumza wala kutoka kimapenzi na mtu yeyote.
“Nitakuwa single milele? Haiwezekani. Nahitaji pia kuwa na mtu wa kuniburudisha,” amesema Cardi.
Ameongeza kuwa baada ya kuachana na nyota wa NFL, Stefon Diggs, ameendelea kufurahia maisha kwa kusafiri, kutoka na marafiki pamoja na kupumzika.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 33 alisema umaarufu wake unamlazimu kuwa makini zaidi katika kuchagua mwenza, akieleza kuwa humchukua muda kuamini na kumpenda mtu.
“Labda naweza kuchagua wanaume bora zaidi, inawezekana. Lakini sitabaki single milele. Maisha ni mazuri, lakini hata moyo wangu unahitaji upendo,” alisema.
Cardi B amehusishwa kimapenzi na nyota wa NFL, Stefon Diggs, na wawili hao walikuwa katika uhusiano wa kusuasua. Mapema mwaka huu, Cardi amesema alipoteza imani katika uhusiano huo na kuamua kuelekeza nguvu zake katika kulea watoto wake, muziki na ziara zake za kimuziki.
Hata hivyo, vyanzo vya karibu na wawili hao vilidai kuwa Diggs alifanya jitihada za kurekebisha uhusiano huo, jambo lililomfanya Cardi kuanza kufikiria upya kuhusu mustakabali wao.




