Nyumbani

TFF yazionya klabu kuhusu vijana wa TDS

DAR ES SALAAM: RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amezionya klabu zinazowasajili wachezaji wanaotoka katika vituo vya Tanzania Development Soccer (TDS) kufuata utaratibu uliowekwa, akisisitiza kuwa vijana hao wanapaswa kulindwa ili wasitumike vibaya katika masuala ya mikataba.

Katika mkutano na waandishi wa Habari leo Karia amesema wachezaji wanaolelewa katika vituo vya TDS chini ya umri wa miaka 17 huwa chini ya mfumo maalumu wa maendeleo, na baada ya kufikisha umri wa miaka 17 na kuhitimu, huruhusiwa kwenda kwenye klabu au sehemu nyingine kwa ajili ya kuendeleza taaluma zao.

Amesema baadhi ya klabu tayari zimeanza kuwasiliana na wachezaji waliopo TDS na hata kuwapatia mikataba, jambo ambalo TFF imeliona na kutoa tahadhari.

“Tunawataka wale watoto wasichezewe. Wana kazi ya taifa na tunataka kuifanya,” amesema Karia.

Amesema TFF haingilii mikataba ya klabu na wachezaji, lakini historia ya mchezaji itaonekana kwenye hati ya mchezaji, hivyo itafahamika ni muda gani aliutumia TDS na alikwenda klabu gani baada ya kuhitimu.

Amesema vijana wengi wanaotamba katika mfumo wa sasa wa soka la Tanzania wamepitia TDS, huku baadhi yao tayari wakianza kuchukuliwa na klabu mbalimbali.

Karia amesema TFF imekuwa ikitembelea mikoa mbalimbali kutafuta vipaji, hivyo si sahihi kwa klabu kudai umiliki wa mchezaji kwa sababu tu imemkuta akiwa katika eneo fulani, wakati mchezaji huyo tayari yuko kwenye mfumo.

Amesema mfumo wa TDS umewekwa kwa ajili ya kuibua na kukuza vipaji kabla ya vijana hao kuingia katika soka la ushindani wa juu.

Related Articles

Back to top button